Asubuhi na mapema, Bw. Nadama aliondoka na familia yake kuelekea kule ambako mkewe alikuwa amemweleza. Mle garini wote walikuwa kimya. Bw. Nadama alikuwa akiwazia kipi kingetokea walikokuwa wanaelekew; Iwapo Bw.Mhifadhi angemwaga mtama penye kuku wengi, alishindwa ambapo angeficha uso wake asionekane kwa familia yake tena.
Labibu alipokuwa ameketi alikuwa akijipa imani kuwa walikokuwa wanaenda ndiko ambako wangepata suluhu ya janga ambalo lilikuwa likimkumba usiku kucha. Kile ambacho alikuwa akifanya kila asubuhi ni kupiga dua mbele ya Mungu wake.
"Don't be stressed up darling," Bi. Tabasuri alimtuliza, "we are going to have a solution."
"Una hakika mama?!"
"Ndiyo mwanangu, usiwe na shaka."
"Unamwambia asiwe na shaka, kwani huyo mhubiri ni Mungu ndiposa uwe na uhakika hivyo," Bw. Nadama aliingilia kati.
"Ah! Mume wangu, ni mara ngapi tumepata msaada na utatuzi wa shida zetu kutoka kwake!"
"Mi' simwamini kabisa, anaonekana mkorofi na mwenye ukaidi, mjuaji wa vyote."
"Kweli mwanadamu hana fadhila, hata ukitenda jambo zuri namna gani lazima utapata ambao watakereka nalo, ushasahau ajali uliyosababisha pale sokoni kwamba ndiye alitoa payslip yake kukulipia rufaa kwa moyo mkunjufu kukusaidia, kama siye tungetoa wapi?!"
"Alitaka umaarufu kutoka kwa halaiki, unajuaje labda ndiye alipanga kitoto hicho kipite hapo. Jiulize, kwa nini pekee yake akajitolea kufidia, kwani watu wenye mifuko mizito kuliko yake hawakuwepo! Hata kampuni yenyewe ingelipa, naye kwa sababu ya kiherehere akajitokeza kujifanya aliyenavyo."
"He sacrificed up his payslip for you, but even you are not grateful for that," Labibu alimwambia babake.
"Sacrificed up, kwani ye' ni Yesu ndo ajotolee kwa ajili yangu!" Babake aliuliza kwa kiburi, "did I ask him to?!"
Bi. Tabasuri pale alipokuwa amekaa, alitikisa kichwa kwa maneno ambayo yalikuwa yanamtoka mumewe.
Safari iliendelea kwa kimya mpaka dereva alipofunga breki mbele ya kibanda kimoja. Gari liliposimama, Labibu ndiye alikuwa wa Kwanza kutua mguu wake kwa mchanga wa ugenini.
"Shuka tuondoke mume wangu, ah mume wangu," Bi. Tabasuri alimwambia baada ya kuona hakuna dalili zozote za kushuka kwa mwenzake.
"Kwani nimekushika?! We nenda, si lazima tuandamane sote."
"Lakini tumekuja pamoja."
Baada ya maneno yale, mkewe alishuka wakaanza kuondoka na mwanawe, sekunde kadha zilipita kisha mwenzao akafungua mlango tayari kuwafuata, lakini akasita kidogo kwa sababu ya mawazo yaliyokuwa yanamsumbua.
"Potelea mbali," alijiambia kwa ujasiri kisha akaanza kuwafuata.
Walipofikia kile kibanda walimpata Bi. Alizeti, mkewe Bw. Mhifadhi akifagia nje ya kiambo chake. Bw. Nadama alikuwa anatembea polepole kama aliyetembea juu ya miiba.
"Siku njema huonekana asubuhi," Bi. Alizeti aliamba akimkumbatia Bi. Tabasuri, "karibuni."
"Lakini labda si hivyo, inaweza ikaanza vema na kukamilika vibaya."
Bw. Mhifadhi aliposikia sauti ya kondoo wake aliyekuwa amepotea kwa muda alitoka nje na taulo kiunoni, ulikuwa mwendo wa saa mbili za asubuhi.
"Mgeni njoo mwenyeji apone," aliwaamkua kwa furaha, "nilikuwa napanga kuja kutembea kwako siku moja, umepotea kwa muda mpaka nikawa na dukuduku moyoni."
"Ni kweli usemayo, lakini si kwa kupenda, ni kwa sababu ya matatizo madogomadogo ya hapa na pale," Bi. Tabasuri alimjibu kwa huzuni.
Pale mlangoni Bw.Mhifadhi alianza kuwachunguza mmoja baada ya mwingine; wa Kwanza alikuwa Labibu aliyekuwa amekaa upande wa kushoto wa mamake, alionekana asiye na furaha, tena ambaye anasumbuliwa na kitu ambacho kilimzidia nguvu. Wa pili alimwangalia mamake Labibu, alionekana mwenye mawazo, kisha mwishowe alimwangalia Bw. Nadama aliyekuwa amesimama hatua kadhaa nyuma ya familia yake, dhamira zake zilimuonyesha kwamba kuna kitu ambacho alijaribu kuficha kutoka kwa familia yake. Alipomwangalia usoni, mwenzake aliangalia chini, alikuwa na sura ya wasiwasi.
"Kari..."
"Ah! We nawe, nenda bafuni kwanza kisha ubadili hayo mavazi yako, leo wako papa hapa, hawatoki," mkewe alimkatiza.
Bi. Alizeti kwa furaha, aliwaongoza wenzake mpaka chini ya mzambarau ambapo miale ya just ilikuwa imepenya katikati ya majani. Labibu aliangaza macho kutoka pale alipokuwa ameketi akafurahia kila alichoona.
Miale ya just ilipotua juu ya nyasi zilizokuwa zimefyekwa ilifanya zikang'aa kama dhahabu.
"Hata kama ni kugoma kutuonekania, si kwa kiwango hicho mpaka nikafikiri umepatwa na maluja," Bi. Alizeti alimtania mamake Labibu.
"Si kupenda kwangu kuwepo kwa hali hiyo," Bi. Tabasuri alimjibu akitikisa kichwa kama mtu aliyekuwa anajaribu kujiondolea mawazo.
"Nikafikiri hata labda umepatwa na maafa!"
"Hata hivyo, mimi naamini kwamba kitu ambacho mtu huthamini sana katika maisha yake hata kikiondoka huwa pamoja naye kiroho kwa sababu huwa kama sehemu ya mwili wake."
"Ni kweli, lakini...," Bi. Alizeti alikata maneno yake akamwangalia Labibu.
Hata pale alipokuwa ameketi, mbele yake alikuwa anawaona wale watu ambao alikuwa amewaona katika ndoto zake mara kwa mara. Alitaka kukimbia lakini akashindwa. Zile ndoto za kishirikina zilikuwa zimefanya akapoteza furaha, hata asione tena haja ya kuishi.
"Labibu amekuwa mnyamavu kweli, hii si tabia yake," mwenyeji wao alitamka akimgusa kwa bega lake la kulia.
Aliyeguswa alishtuka kama mtu ambaye alikuwa usingizini, ule mshituko ulimshtua Bi. Alizeti nusra aanguke kutoka kitini.
"Uko salama binti yangu?!"
"Ndiyo, 'mi niko sawa," Labibu alimjibu akikwepa macho yake.
"Usiwe muongo mwanangu," mamake alimuonya akitokwa na chozi katika jicho lake la kulia, alimgeukia mwenyeji wao na kumwangalia ya huruma, "mwanangu anasumbuliwa na ndoto ambazo si za kawaida, mara watu waliovalia maguo mekundu wanawakimbiza msituni...babake anakamatwa na watu hao tayari kuuwawa... lakini hustuka kutoka usingizini na kutoa ukemi. Cha kushangaza zaidi ni kuwa, kati ya wauaji mmoja wao ni Bw. Vura amabaye huinua upanga tayari kumuangamiza."
Kisa kile kiliwaacha waliosimuliwa vinywa wazi, ilikuwa ndoto ya kutisha. Bw. Nadama alikuwa ameketi mbali nao kama mtu ambaye hakuwa na shughuli yoyote na kikao chao.
Bw. Mhifadhi alitikisa kichwa baada ya maelezo ya mamake Labibu.
"Nilijua lazima mambo kama haya yatatokea," aliwaambia baada ya sekunde kadha.
Wale watatu; Bi. Tabasuri, Labibu na mkewe walimwangalia kwa mshangao, walishindwa na kile alichomanisha, wote kwa pamoja wakageuka na kumwangalia Bw. Nadama aliyekuwa ameketi nyuma yao.
"Unamaanisha nini ukisema nilijua mambo kama haya yatatokea," mkewe alimuuliza baada ya kushindwa kujizuia.
"Muulizeni Bw. Nadama, bila shaka anajua ninachomaanisha."
"Sa' mimi katika maongezi yenu nikaingilia wapi!" Bw. Nadama aliuliza bila kumkusudia yeyote, lakini akiwa amemwangalia mnenaji kwa macho ya chuki.
Alijua ambako Bw. Mhifadhi alikuwa anaelekea, alijua sekunde yoyote chungu alichokuwa ameshikilia kwa mikono mitatu kingeanguka na vilivyomo kuenea, kitu ambacho hakutaka kitokee.
Bi. Tabasuri alianza kujishuku kwa sababu alizojua mwenyewe, Labibu baada ya Bw. Mhifadhi kumtaja babake, dukuduku ilimzidia moyoni.
Bw. Mhifadhi alijua anahitaji kuwa jasiri kupita kiasi ili kuiondoa familia ile katika giza na kuiweka pahali pema. Alikuwa ashasikia wengi ambao waliungulia katika moto wa dharau wakijaribu kuelimisha na kutahadharisha jamii kuhusu maovu yaliyokuwa yakiendelezwa na muungano huo wa siri.
"Kumbuka ulikuwa mwendo wa saa sita za mchana, siku ya Jumamosi," Bw. Mhifadhi alianza kuelezea, "mchana peupe ulipojiingiza katika agano na shetani."
"Unazungumzia nini nisichoelewa," Bw. Nadama aliteta akionekana mwenye wasiwasi.
"Usijifanye asiyefahamu ninachozungumzia, ulikuwa wakati ambapo jua lilikuwa utosini, jicho la Mungu likiwaangazia wote, uliamua kuingiza pabaya nafsi na roho za familia yako bila kujali," alimwaga ukweli mbele ya kikao chake, "methali tamaa mbele mauti nyuma haikuwa na maana kwako, ukaamua kufumba macho kumuasi Mungu mchana.
"I...can see...," Bw. Nadama alikuwa ameshikwa na kigugumizi kwa sababu ya hasira ikiyompanda, "unajiita mhubiri, huna hata haya kunena uongo mbele ya waumini wako."
"Ambayo nimenena si uongo unavyosema, ni ukweli bila doa lolote."
Wale watatu walikuwa wameshanga zaidi baada ya kusikia maneno ya Bw. Mhifadhi. Labibu na mamake pale walipokuwa walijiona wamo katika ndoto, kweli waliupata lakini hawakuamini. Bi. Alizeti naye kwa upande wake alijua ambayo mumewe alinena yalikuwa ukweli, lakini naye vilevile hakuamini.
Kwa hasira Bw. Nadama alimgeukia mkewe.
"Unajionea sasa ujinga ambao ulinileta kuganya, mhubiri wenu wa uongo, hizo ndoto zako wapelekee unaoita kondoo kanisani, na kweli ni kondoo," alitamka kwa hasira na kusukuma kiti tayari kuondoka.
"Lakini unaenda wapi mume wangu," mkewe alimuuliza akifikia koti lake kumzuia, "huwezi ukaondoka na kutuacha katikati ya kikao."
"Unataka niondoke mwanzoni mwa kikao sio! Hebu nipishe mie, nyi muendelee na kikao chenu cha kijinga."
Bi. Tabasuri akiwa bado amemshikilia, alihisi uzito shavuni uliomwangusha akawa hana budi kumuachilia mwenda zake. Bw. Nadama alipofikia gari lake, aliingia akatifua vumbi na kuondoka. Mkewe alimwangalia asijue cha kufanya.
"Siku moja Mungu atamfumbua macho aone mwenyewe uamuzi aliofanya," Bw. Mhifadhi alinena akimsaidia Bi. Tabasuri kufikia kiti chake kisha akaondoka.
Wale wengine walisalia pale wakiwazia kile ambacho kilikuwa kimetokea. Mamake Labibu hakuwa ameamini kwamba mumewe wa miaka thelathini ndiye aliyempiga kofi.
****
Bw. Nadama hata baada ya kuondoka mahali pale alikuwa anasikia sauti ya Bw. Mhifadhi maskioni na yale ambayo alikuwa amemwambia.
Alikuwa amechanganyikiwa kwa yale ambayo alikuwa amesikia alikotoka, alipofika njia panda mjini Maizi alisimama, hakujua arejee nyumbani kwake au aelekee hotelini ambapo angekutana na rafikiye.
"Sir, you are delaying some of us!" Sauti ya kike ilimshtua kutoka pale karibu na mlango wa gari lake, "am rushing for an important meeting."
"Samahani dada," alimuomba radhi yule mwanadada, "am confused and I've headache."
"Basi hufai kuwa barabarani kwa sababu unaweza ukasababisha ajali na hata labda kupoteza maisha. Inafaa ufike hospitali."
Hata yale maneno hakuyasikia, alipoangalia nyuma aliona msongamano wa magari aliokuwa amesababisha, akaangalia saa yake kisha akaondoka kuelekea hotelini.
"Nimesimama kwa dakika tano bila kujielewa," alisema mkono ukifikia kiti cha abiria.
Alitarajia kumgusa mkewe lakini mkono wake ukafikia godoro la gari, alitikisa kichwa kwa vitendo ambavyo alikuwa anafanya. Aliona ni kama alikuwa anapagawa kwa sababu ya mawazo, alionekana mtulivu lakini hakuwa na amani akilini kila alipokumbuka alichofanya akitarajia kiwe siri kilikuwa sasa katika hatari ya kuenea angani ambapo kingemuonekania kila mtu.
"Kumbuka ulikuwa mwendo wa saa sita za mchana siku ya Jumamosi ulipojiingiza katika agano na shetani," aliridia maneno ya mhubiri wake wa awali.
Kila neno ambalo Bw. Mhifadhi alikuwa amesema lilikuwa la ukweli, lakini hata mwenyewe hakuwa ametarajia alilotenda kujulikana kwa yeyote.
"Lakini alijua vipi mambo haya wakati yalifanyika?," alijiuliza, "au ashaambiwa na Bw. Vura...ha...pana, sitaraji kwa sababu hata mwenyewe alinisisitizia nisifikiri kutamka lolote kuhusu siku hiyo."
Safari yake ilimchukua masaa mawili kabla hajatia nanga mbele ya hoteli moja kubwa ya kifahari, alimpaa jamaa moja funguo zake za gari ampelekee maegeshoni, kisha mwenyewe akaondoka mbio.
Alipofika ndani ya jumba, alikaribishwa kwa harufu nzuri za vyakula ambavyo vilikuwa vinaandaliwa.
"Niko upande huu bwanangu," alisikia jamaa mmoja akimpazia sauti kutoka katika pembe moja ya jumba lile.
Alipogeuka alimuona rafikiye, akaenda na kuketi . Meza yenyewe ilikuwa ishachafuliwa na vileo vya kila aina na vinywaji vya bei ghali.
"Mbona ukachelewa hivi?" Bw. Vura alimuuliza akimimina maziwa ndani ya bilauri na kumkabidhi, "tuliagana kupatana saa tano, lakini saa hizi ni saa nane."
"Nilikuwa na shughuli ndogondogo za nyumbani ambazo zilinilazimu kukamilisha kabla sijafanya chochote."
"Shughuli zipi ambazo hazina majina."
Bw. Nadama pale alipokuwa alimwangalia mwenzake usoni barabara na kuwazia kile ambacho kilikuwa kimetokea, alitaka kumueleza lakini baada yake kukumbuka kile kiapo aliapa kutomwambia kwa sababu alijua atashutumiwa.
"Nilikuwa namshughulikia mwanangu arudi shule," alimdanganya mwenzake.
"Ah! Jambo dogo kama hilo, ungenijuza tu bila mvutano wowote, ulikuwa unanitia shaka moyoni."
"Usiwe na shaka, ni madogo tu hivyo."
Bw. Vura bila kupoteza wakati alianza kumsimulia mwenzake kuhusu yule mteja ambaye alikuwa amemkuta katika ofisi moja ya kampuni zake. Alimwambia jinsi alikuwa amekipangia kile kizee msiba ambao ungeathiri maisha yake yote kwa sababu ya kudai malipo yake. Fikra za mwenzake zilikuwa mbali sana na kiwiliwili chake, yale maelezo aliyokuwa anapewa na muhibu wake alikuwa anang'amua neno moja katika kila sentensi tatu.
"Wewe unanishauri vipi rafiki yangu?" Bw. Vura alimuuliza mwenzake baada ya kumaliza alichokuwa anasimulia, "Bw. Siga anasema nimlipe."
"Hakuna haja ya kuwepo ubishi wakati wa malipo, apewe malipo yake," Bw. Nadama alimjibu kwa sauti ya chini tena yenye unyenyekevu.
"Sioni haja ya kutupa hela baharini kama ambazo hazina matumizi maalum!"
"Lakini kulipa pia ni kazi, mtu anafaa kulipwa ujira wake baada ya kumaliza alichokuwa anafanya, au alikosea popote?!"
"Hapana."
"Basi kama hakukosea popote apewe kinachofaa."
"Lakini hata kizee chenyewe hakina mbele wala nyuma, hakina ulimi wa ushawishi."
"Hata kama hakina pa kuegemeza ubavu, unahatarisha kuporomosha kampuni yako iwapo utaenda kortini kisha mambo yawe kinyume na matarajio yako," Bw. Nadama alimkazia.
Baada ya ubishi kati yao wa dakika tano hivi, Bw. Vura alinyamaza kwa hasira, siku zote aliona uamuzi wake ndio uliofaa kuliko wa mtu yeyote aliyekuwa karibu yake. Pale ambapo rafikiye alikuwa amekaa, mwanga kuhusu aliyoambiwa na Bw. Mhifadhi ulimjia.
"Lakini naona uamuzi wangu ukiwa sawa, sioni jinsi ya siafu na bidii yake ataweza kuangusha mbuyu," Bw. Vura alimwambia mwenzake, "tena si jeshi lake, bali siafu mmoja tu, hata huyu ndege anaweza kumdona."
"Kwa nini ukaniita mahali hapa?," Bw. Nadama alimuuliza.
"Nilikuita unishauri, lakini hata nao ushauri wako hauna mashiko kama hapo awali."
"Basi kama ulijua uamuzi wako siku zote ni sawa hungeniita, ungejitatulia shida zako mwenyewe," Bw. Nadama alimwambia akiinuka kwa hasira, "kwaheri."
"Nadama! Usiwe hivyo bwana, huo umekuwa utani."
Bw. Nadama alimsikia mwenzake akimsihi, lakini akakata kauli yake na kuendeleza mwendo, kule nyuma alikotoka mwenzake alianza kumuonea gere.
"Si kawaida yake kughairi chochote ninachomwambia," Bw. Vura alijiambia kwa sauti ya chini pale alipokuwa ameketi.
Alianza kuvuta picha wakati ambapo walikuwa na mazungumzo na rafikiye, alikumbuka jinsi mwenzake alikuwa amekazia macho ukutani kama mtu ambaye alikuwa anaangalia kitu kwa makini zaidi, licha ya kuwa walikuwa na mazungumzo pale mezani.
Ameonekana mwenye fikra...ama kuna kitu ambacho kimetokea lakini hataki kunipa taarifa...," alijiuliza midomo ikimcheza kwa hasira, "ama amevunja ahadi aliyotoa mwenyewe...ndo...ni hicho tu kinachoweza kumfanya awe namna hiyo."
Fikra hizo zilipompitia akilini, aliinuka mara moja kochini kama aliyedungwa kwa sindano, alipokuwa anachukua koti lake, kwa bahati mbaya akigonga glasi ya maziwa ikaanguka na kuvunjika. Kelele ya kuvunjika kwa glasi kuliwashitua wateja wenzake, wote wakageuka na kumwangalia lakini naye akajitia hamnazo na kuondoka kama mtu ambaye hajatenda maudhi yoyote.