Bw. Nadama alipofika nyumbani kwake na kukosa mkewe Bi.Tabasuri, alipata nafuu moyoni, juma moja lilikuwa lishapita tangu walipomtembelea mhubiri na yale mambo kutibuliwa.
"Nitapumzika saa nzima kisha niondoke kabla hajafika na maswali yake," alijiambia akilegeza tai yake na kuingia sebuleni.
Yalikuwa masaa ya adhuhuri alipofika nyumbani baada ya kutoka kazini, alipumzika kochini akifikiri kuhusu biashara zake zilivyokuwa zinanawiri kila jua lilipofunga kope zake.
Alipokaa kwa ghafla macho yake yalitua juu ya picha iliuyokuwa imepigwa na mwanawe Guta kwa ghafla alianza kutokwa na machozi. Alipoiangalia tena aliona ni kama mwanawe alikuwa anamuita, aliamka na kuitoa ukutani kisha akaifunika juu ya kabati.
Picha ile ilimkumbusha mambo ya ajabu ambayo yalikuwa yametokea kabla mwanawe hajaaga dunia.
Alikuwa akiota ndoto ile ile iliyomsumbua Labibu, akawa mtu wa kushtuka na kupiga ukemi wakati wowote. Alikuwa ni kama aliyekuwa anaona visivyoonekana kwa wengine, siku mbili kabla kifo chake alianza kumlilia mamake kuwa anaumwa na kichwa.
Alipelekwa hospitali ya kitaifa ya Gunga, huko joto lilimzidia mwili mzima, madaktari walimshughulikua kwa jino na ukucha, wagonjwa wengine wakawa hawahudumiwi kwa sababu yake.
Mwenyewe alikuwa kando ya kitanda cha mwanawe wakati huu wote, baada ya mgonjwa wake kupigania maisha yake bila mafanikio, siku ya tatu mwendo wa saa sita na nusu aliipa dunia mkono wa buriani.
Siku ya mazishi yake pia kisa cha muujiza kikatokea ambapo waombolezaji walivamiwa na nyuki wakatundika miguu begani kila mmoja na kuwaacha wazazi na maiti yao.
Nyuki waliingia mpaka ndani ya jeneza walipomaliza dakika tano kisha wakaondoka. Mazishi yaliahirisha yakafanyika baada ya siku mbili.
Haya yote yakitokea alikuwa kimya, mkewe akawa ndiye mzungumzi wake. Kisa nyuki matangani kikaenea kwa vinywa vya wadogo na wakubwa pale mtaani lakini baada ya wiki mbili hivi kikasahaulika.
Alipokuwa amepumzika haya yote yakimpitia akilini aliskia mlango ukifunguliwa, akafuta machozi kwa haraka.
"Shikamoo mume wangu," mkewe aliyekuwa ameingia alimuamkua akimbusu.
"Marahaba."
"Nimeona gari maegeshoni nikashtuka."
"Nilijua, hilo si la kuongelea!"
"We nawe. Nilishtuka kwa sababu sijazoea kukuona ukirudi nyumbani masaa ya utosini."
"Umezoea kuniona nikija masaa ya wayoni sio."
Bila kujibu mkewe alicheka kisha akaondoka na kuelekea jikoni kuandaa chakula lakini hata naye hukuwa na amani baada ya kumuona mumewe majira hayo, alikuwa ashaona alama za michirizi ya macho usoni mwake lakini hakuuliza kuhofia jibu ambalo angepokea.
"Karibu mezani," akimkaribisha mumewe baada ya kuandaa chakula mezani.
"Na Labibu yuko wapi?"
"Ah! We nawe, yuko shule. Ushasahau kuwa mwanao anafaa awe shuleni! Jiondolee mawazo."
Mumewe alitikisa kichwa kwa haraka, wakaanza kula kwa pamoja, lakini baada ya mkewe kutua kinywani vijiko viwili vya wali, alimwangalia.
"Lakini mume wangu, unaweza angalau kunielezaa kwa nini uko nyumbani masaa haya ya kazi," Bi.Tabasuri alianza.
"Nimekuwa kupumzika kidogo kuondoa mawazo, huko Kuna kelele, kazi nyingi ambapo huna hata sekunde moja ya mapozi."
"Ni vema kupumzika kuliko kujiwekea shughuli chungu nzima wakati huna hamu ya kuzifanya."
"Nimeamua kuwa na wangu wa tokea zamani mchana huu angalau atanipunguzia mawazo," Bw.Nadama alimwambia.
Mkewe alitabasamu, kwa utaratibu akamwangalia kwa macho ya mahaba, alitaka kuanzisha mazungumzo yake ya siku baada ya siku nyingi lakini akasita.
Hakutaka tena amuudhi mumewe kwa wakati huo kwa sababu alijua ataachiwa meza mzima. Naye maneno aliyokuwa ameskia kutoka kwa Bw. Mhifadhi yalimuumiza moyoni, ingawa hakuwa na hakika iwapo ya yalikuwa ya kweli au yalikuwa uvumi ambao mtumishi wao alitoa kwa wanakijiji.
"Mume wangu nataka nikuulize swali, ila naomba usininyamazie. Ila nipe jibu lolote," alimuanzia mwenzake.
"Bora yasiwe hayo mambo ya kawaida," alionywa hata kabla hajauliza.
"Lazima nipate mwanga hata kama ni hafifu kutoka kwako, utaniwezesha kuona tunakoelekea."
Mumewe alimwangalia kwa macho ya kuogofya hadi akahofia kwamba labda kitu kibaya kinaweza kutendeka wakati wowote, lakini naye kwa woga akamkazia yake bila kupepesa. Bw. Nadama alianza kufikiri atakavyojitetea kwa swali lolote ambalo ataulizwa.
"Ni kweli yaliyosemwa na Bw. Mhifadhi juu yako ama...?"
"Nimekuonya sasa hivi lakini wewe ungali kusukuma mshale moyoni kutoka mwenzako alipowaachia. Unaanza kumea pombe, sijui ni za plastiki, dhahabu ama za fedha," mumewe alimzomea akiwa na nia kumtisha asiulize swali jingine, " au ndo kiburi mnachofunzana huko saluni unakoenda kukutana na mashangingi wenzako."
"Nimekuuliza kwa upole mume wangu, kwa nini kunikaripia?!"
"Unasema kukukaripia, mambo hayo nilikwambia yabaki kuko huko unakokutana na pasta wako wa uongo na sitaki tena kuyasikia katika nyumba hii."
"Sijasikia kwamba amemtenda mtu yeyote maudhi katika kijiji hiki," Bi. Tabasuri alimtetea mhubiri wao, "we' ndiye wa kwanza kusikia ukitoa malalamishi juu yake kwa mwongo mmoja ambao nimemfahamu."
"Unaamini kila asemalo kwa sababu ni mtumishi wa Mungu!"
"Ndiyo, maneno yake huyaamino kwa asilimia kubwa, lakini hayo aliyosema juu yako yalinitia kiwewe."
"Ulimwamini?!"
"Hapana."
"Basi usiamini kamwe, narudia tena maneno yangu kwamba sitaki kuyasikia. Nadhani umenisikia."
"Ndiyo, laki..."
"Kumbuka, watu wawili hawasimami kidato kimoja ngazini," alimuonya mkewe, "kwa sababu uzani wao huenda ukakilemea, lazima mmoja atakuwa juu ya mwingine."
"Kwa dakika moja wakisimama bila kucheza kinaweza kikawafaa, na sioni haja yako kunishusha wakati nataka kujua ukweli."
"Ukweli upi?!"
"Ukweli kuhusu yaliyonenwa na Bw. Mhifadhi juu yako."
"Utaamini chochote nitakachokuambia, sio?," Bw. Nadama alimuuliza akipanga jinsi ya kumdanganya, "bora kitoke kinywani mwangu."
"Ndiyo, lakini."
"Ulakini wako siupendi kabisa, ukweli ni kuwa mimi sijajihusisha na chochote ambacho mhubiri wako alisema."
Japo Bi. Tabasuri alijua anadanganywa, hakusema chochote, wakarudia chakula kilichokuwa kimesahaulika mezani. Bw. Nadama alikuwa akila lakini macho yake yakimkagua mkewe kichinichini, naye Bi. Tabasuri alikuwa amebaki katikati ya wale insi wawili akishindwa yupi alikuwa anampaka mwenzake tope.
"Mume wangu, kwa muda ambao umepita umebadilika si kidogo," alianza tena.
"Nimebadilika nikawa nyani, sokwe au nguruwe?!"
"Simaanishi kimaumbile, bali kitabia na pia jinsi unavyoongea tunapokuwa pamoja. Mara nyingi unanikaripia hata kwa mambo ambayo hayana msingi, yaani hayana maana kabisa."
"Kama nakuzomea kwa sababu ambazo hazina msingi, huwa nakuzomea kwa sababu ambazo zina paa," Bw. Nadama alimjibu kwa dharau, "basi kama hazina msingi mbona usizijengee!"
Bi. Tabasuri alikuwa ameweka kijiko mezani akaanza kumsikiliza manju wake ambaye alikuwa anatoa hoja ambazo kwake ulikuwa ujinga.
"Maongezi yako ni ya kitoto na kijinga kwa wakati mwingi," mkewe aliropoka baada ya kushindwa kuzuia hasira iliyokuwa imejaa moyoni.
"I see, kiburi kimezidi mpaka unanilinganisha na mtoto mdogo, sio?" Bw. Nadama alimuuliza akisukuma kando sahani tayari kumtia adabu.
Kwa haraka Bi. Tabasuri aliinuka akasonga nyuma hatua mbili, alikuwa ameanza kutetemeka kama jani wakati wa kipupwe, alisonga hadi akafikia mlango kisha akamwangalia mumewe. Kutoka kwa macho yake, aliona ufedhuli ambao angetendewa sekunde kadha za mbele.
"I am sorry," aliomba msamaha kumpoza, "nisamehe, sitarudia tena."
"Hukutaka nile chakula chako," Bw. Nadama alimwambia akichukua koti lake kochini tayari kuondoka.
"Lakini ni chetu sote!"
"Chenu na nani! Jua watu unaotangamana nao, si kila mtu anayekujali kwa jina la Mungu ni wa kuaminika, heri shetani unayemjua kuliko malaika usiyemjua, kwaheri," Bw. Nadama alimuonya mkewe kisha akaondoka akionekana aliyeghadhabika.
***
Asubuhi na mapema Bw. Vura aliondoka nyumbani kwake bila hata kustaftahi, mkewe Bi. Adimu alimshawishi angalau apate lakini akaambulia patupu. Alipotoka mlangoni aliangalia saa yake kisha akakunja uso kama aliyesinyikwa na kitu.
"Masaa yaenda mbio namna gani?!" Alijiuliza akiangalia nyuma kumwangalia mkewe aliyekuwa amerudi ndani kumletea koti, "majira hayaniheshimu, tabia gani hii!"
"Muda hauna mwenyewe mume wangu," mkewe alidai akimvisha koti, "sasa unaweza ukazungumza mbele ya watu."
"Tangu nilipokuoa, umeninadhifu kweli, hata huwezi kumruhusu mfalme wa taka akatua kwangu."
"Ni hivyo, mbona niruhusu uchafuke wakati ningalipo, watu watanidharau wakisema siwezi kumtunza mume wangu."
"Kila siku 'mi hupiga magoti na kumshukuru Maulana kwa ajili yako," alimwambia akigeuka na kumbusu, "nisingekuoa, singeoa tena maishani kwa sababu we ndiye chemichemi ya mapenzi yangu."
"Siku zote uongo umejaa mdomoni, ni kama tu wanaume wengine ambao wakiwa na wake zao huwabemba sin haba, lakini mguu unapotoka nje ya malango yao wanawasahau kabisa yale ambayo wamekuwa wakizungumzia na wake zao, hao ni wanafiki."
"Mimi si wao na wala wao si mimi; Mimi ni mwenye mahaba ya kweli kuliko wanaume wote duniani."
"We' ni wa sayari ipi; Zebaki, Zuhura au Mirihi, mimi wanaume wote duniani huwaona kama walaghai," mkewe alimwambia akimtengeneza tai, "miaka hii yote na hujui kufunga tai, aa! We nawe unajishusha zaidi, unafunga kama boi wa mashambani ilhali we ni wa kuheshimika Gunga nzima."
"Sina haja ya kujua wakati kioo changu kingalipo," alimwambia mkewe akiangalia tena saa yake, "ah! Saa moja unusu, unafanya nichelewe kwa hivi vidoido vyako."
Alitimka mbio kutoka alipokuwa amesimama na mkewe kama mtu aliyefukuzwa, mkewe akabaki pale akimwangalia.
Kwa haraka, alifikia mlango wa gari akafungua na kuingia, akatia moto tayari kuondoka.
"Siku njema," mkewe alimpazia sauti kutoka alipokuwa amesimama lakini hajuitikiwa, "nilimwambia akasema namsemea umbea, ashanisahau hata kabla hajatoka ndani ya majengo haya."
Bw. Vura alitoa gari maegeshoni kama mtu aliyekuwa anakimbizwa na kifo, nusra amgonge mlinzi wake.
"We kipofu au!" Alimfokea bawabu, "unaona gari lakini ungali unababaika kama asiyejua la kufanya."
"Pole boss," bawabu aliomba radhi.
"Fungua haraka, sina haja na kunradhi kwako, au ndo zinifungulie lango."
"Hapana."
"Unasubiri nini?."
Bawabu alifungua lango kwa haraka bila kungoja jingine kutoka kwa mwajiri wake. Gari lilitoka kwa kasi akasalia pale akitikisa kichwa, alipokuwa amesimama alimtolea bawabu tabasamu kisha akaingia ndani.
Mlinzi alikuwa mvulana wa miaka kama ishirini na miwili hivi, kando na lango, palijengwa kijumba cha mbao ambapo aliishi kisha kando yake pakajengwa kijumba cha mbwa.
Bw. Vura alipotoka nyumbani kwake alielekea katika kampuni yake.
"Natumai amefanya nilivyomwagiza," alijiambia akipinda kona mkono wake wa kushoto, "au kama ameghairi agizo langu, atanitambua."
Alipofika langoni, alisimama pale dakika tatu bila kuona mlinzi, aliangalia tena saa yake akatikisa kichwa. Alipiga honi kwa nguvu ikatoa sauti I love iyowashtua wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi zao karibu na lango, alipiga mara tano, alipotaka kubonyeza mara ya sita, alimuona mlinzi akija kifua mbele. Alionekana aliyeghadhabishwa na tabia mbi za mgeni wake.
"Hujajua utaratibu wa kumuita afisa sio!" Aliuliza kwa hasira akifungua lango, hakuwa ametambua kwamba aliyempigia kelele alikuwa mwajiri wake, "ingia ndani nikuonyeshe."
Baada ya kufungua lango, alisonga kando kumpisha, alipoangalia gari kwa karibu ndipo alopolitambua. Pale aliposimama alitamani muujiza utendeke apotee asije akakutana na maneno atakayoambiwa.
Bw. Vura aliegesha gari chini ya Mtamando uliokuwa umemea kando, akashuka na kuenda kukutana na yule mlinzi.
"Karibu sir!" Yule mlinzi akimkaribisha kwa uoga, mashavu yake na mkono uliopiga saluti vyote vililoa kwa jasho.
"I see," Bw. Vura alitamka akimwangalia.
"Ndiyo sir!"
"Unaitwa nani."
"Mtu sir!"
"Ndiyo, we ni mtu si burukenge, nataka jina lako."
"Naitwa Kambu Mfarika."
"Uliajiriwa lini?."
"Wiki tatu zimepita sir!"
"Hivi ndivyo ufanyavyo kazi?."
"Ndiyo!"
"Kuchelewesha wateja langoni wakati umeenda ziara zako!"
"Hapana sir!"
"Umekuwa wapi sasa hivi?" Bw. Vura alimuuliza lakini hata kabla hajajibiwa alikuwa ashampiga kofi.
Alianza kumzunguka polepole akimchunguza kila sehemu ya mwili wake, alimuona kama matapishi, akamuona hana maana ndani ya kampani lake. Alipoona firimba iliyoning'inia kwapani alikumbuka alikotokea, lakini kwa haraka akatikisa kichwa kuondoa yale mawazo.
"Sir! One of your workers is sick," alishtuliwa na mfanyakazi mmoja.
"Nimechoshwa na hicho kizungu chenu, sipendi hiyo lugha, hebu rudia kwa lugha ya kitaifa," alimfokea yule mjumbe.
*****
Hakutaka watumishi wake wajue kwamba alikuwa na upungufu kwa lugha ya kimombo, aliamini itikadi iliyozaga Gunga nzima kuwa kiingereza kilifika kwa meli kutoka Ulaya, meli ilipotia nanga, wachache waliobahatika kukiona na kukigusa ndio waliofaidika nacho kabla hakijasafirishwa kwa garimoshi mpaka nchi bara ambako pia wachache waliokuwa navyo ndio waliofaidika na wengine wakasalia katika giza totoro. Aliamini maneno hayo mpaka alipofika shuleni alijaribu kuking'ang'ania lakini kikampiga chenga mpaka alipojifanya mtoro wa shule.
"Nasema hivi bwanangu, mwenzetu pale ni mgonjwa na tunahitaji msaada wako," yule mfanyakazi aliomba.
"Msaada wangu?!"
"Ndiyo."
"Kwani mi' Mungu ndo muhitaji msaada wangu," Bw. Vura alimgeukia mara moja, "mpelekeni hospitali."
"Tuna upungufu kifedha."
"Sasa unataka nikusaidie vipi?!"
"Utukope, tukipata mshahara tutalipa."
"Kwani mi' benki!"
"Hapana, lakini wewe ndiye bosi wetu. Kwenda benki kutschukua muda na huenda tukampoteza.'
"Nafikiri mna kikundi ambapo huekeza pesa zenu kila mwisho wa mwezi."
"Ndiyo, lakini hatuna wakati, huwa anaugua ugonjwa wa kisukari."
Bw. Vura aligeuka kumwangalia mzee aliyekuwa anazungumziwa akamuona anapumua kwa nguvu kama aliyeekewa nanga kifuani. Akilini mwake, alifikiri walikuwa wanamchezea shere wapate wakati wa kupumzika.
Alimgeukia tena mlinzi aliyesimama kama sanamu.
"Nawe ulikuwa unatoka wapi?," alirudia tena swali ambalo alikuwa amemuuliza hapo awali.
"Nilikuwa natoka kwa meneja sir."
"Usirudie kosa kama hilo la kuacha lango bila muwajibikaji wake."
"Ndiyo sir!" Mlinzi aliitikia akitoka mbio kwenda kufunga lango lililokuwa limeachwa wazi.
Alianza kuondoka kuelekea ofisini mwa meneja wake kwa haraka, alikuwa ashasahau mazungumzo yaliyokuwepo Kati yake na yule mwanadada. Mjumbe alimwangalia kwa mshangao alivyokuwa anaondoka akafikiri labda ni madharau.
"Sir! I've asked you for some money," alimpazia sauti kwa heshima.
"Nawe ni nani kumtetea," alimfokea akirudi alikokuwa ametoka huku amemnyoshea kidole, "'we mwakilishi wa wafanyakazi?!"
"Hapana boss."
"Then, kwa nini unamtetea!"
"Ni mwenzangu hapa kazini, lazima niwajibike kwa ajili yake ninapohitajika."
"Kwa nini wengine wasiwajibike isipokuwa wewe."
"Wote wanakuogopa bwana wangu."
"Wananiogopa na kuniheshimu kwa wakati mmoja," Bw. Vura a little alijiambia kwa madaha, "basi, kama wananiogopa, kwa nini nawe hujafuata sifa yao."
"Siwezi kumuogopa mwanadamu mwenzangu, ila namheshimu."
"Unaitwa nani?."
"Arina Kilelecha."
"We mrembo sio," Bw. Vura alimwambia akinyosha mkono kumgusa kifuani.
"Bwanangu, mimi ni mke wa mtu!" Arina alishtuka akaruka nyuma kumuondokea nduli yule.
Bw. Vura alimwangalia kwa kijicho kisha akatua kibeti chake mfukoni na kuanza kukagua hela zake, baada ya sekunde kadha alichomoa noti ya shilingi ishirini akamtupia Arina miguuni.
"Mpelekeni hospitali, kisha atakatwa mshahara wake kunifidia," alitoa agizo.
"Hata hazi..."
"Hata hazitoshi, toa mfukoni mwako zinazotosha. Nanyi munaangalia nini? Mnafikiri hii filamu."
Aliondoka akionekana aliyeghadhabika si kidogo, wengi kati ya wale wafanyakazi walikuwa washanaswa katika mtego wake ndiposa mkatao wa Arina ulifanya moyo wake ukalia machozi ya unyonge.