SURA YA NNE

Bw. Vura aliingia ofisini kwa kishindo bila kubisha, Bw. Siga alipokuwa alipigwa na butwa kumuona bosi wake katika hali hiyo. Alikuwa amezoea kumuona amenuna lakini si kwa kiasi hicho, hata bila kukaribishwa alivuta kiti akaketi, kichwa kilizama mikononi.

"Kuna chochote kibaya kimetokea?," Bw. Siga alimuuliza kwa upole baada ya kuona hali yake.

"Nawe uonavyo! Kuna baya au la!"

"Aaah! Mi' sijui utokako na basi sijui kama ambako umetoka ni salama, unaonekana asiye sawa."

"Umegonga ndipo, siko sawa kabisa," Bw. Vura alimjibu akiinua kichwa.

Kwa sababu ya uoga aliohisi baada ya kumwangalia bosi wake machoni, alikatiza maswali yake ambayo mwenzake aliyaona ya kijinga. Macho ya Bw. Vura yalikuwa na wekundu wa pichi.

"Natumai umefanya nilivyokwagiza kabla sijaondoka mara ya mwisho," Bw. Vura alimkumbusha.

"Hatujaamkuana," Bw. Siga alimkumbusha akimnyoshea mkono.

"Sina haja na salamu zako," alimwambia akiusukuma mkono wake kwa dharau.

Mwenzake alimwangalia kwa sekunde kadha akamcheka moyoni, naye Bw. Vura alikuwa amemwangalia akingojea jibu kwa swali alilomuuliza.

"Nasubiria jibu lako," Bw. Vura alimshtua mwenzake.

"Ndiyo, laki..."

"Lakini tena nini, kama umefanya nilivyokwagiza mambo safi."

"Nilimuahidi aje leo apate malipo yake."

"Malipo yake!"

"Ndiyo."

"Yatoke wapi?!"

Bw. Siga alitikisa kichwa kwa maswali ya mwenzake, alijiona heri kumliko. Aliona mkurugenzi wake ashawachukua wafanyabiashara wenza kama vinyangarika.

"Nisikilize kwa makini, meli inaposafiri baharini hupambana na mawimbi na wanyama wengine wakubwa, lakini vinyama vidogovidogo huvipitia bila tashwishi yoyote."

"Kumbuka hadith ya ndovu na nyuki. Ndovu kwa ukubwa wake alimdharau mwenzake lakini akapitia machungu baadae."

"Unanichukulia vipi ndo unisimulie hadith za paukwa pakawa, hizo ni hadith tu za kubuniwa, kutokea lini ukamsikia ndovu akinena."

"Hata kama ni hadithi, mambo hayo hutokea."

"Hutokea!"

"Ndiyo."

"Lakini si kwangu, mtu ambaye hana cha kuitwa chake atani..."

Alikatizwa kwa mbisho uliobishwa mlangoni, wote wakaangaliana kanakwamba wanaulizana "ni nani".

Wote walinyamaza kama maji ya mtungi, kila mmoja akitaka mwenzake aitikie mbisho. Baada ya kama dakika mbili hivi ndipo Bw. Siga alipokumbuka alivyokuwa amemwalika yule mzee ofisini siku hiyo.

"Karibu ndani," akimkaribisha mgeni wake.

Bw. Vura alipomuona tena yule mzee, aliona kufilisika kunambishia mlango, kitu ambacho hakutaka kitokee katika maisha yake.

"Unafanya nini hapa?" alimuuliza yule mzee akimnyoshea kidole karibu kumdunga jicho.

"Mwanangu, dunia ni duara, ipeleke polepole."

"Ndiyo, najua, nani akakwambia ni mraba?!?" alimuuliza kwa dharau, "wacha niwe wazi sasa hivi, hizo hela sikupi ng'o, hata mtu atoke ahera au mbinguni kwa ajili yako, hutaona hata shilingi."

Bw. Vura alimwaga mtama peupe bila kuficha, japo mwenzake alijaribu kumpoza lakini hakufaulu. Baada ya maneno yale, pale ndani kwa ghafla palizuka rabsha kati ya watu watatu, kisha kwa ghafla akaingia kijana mmoja na kumkwidi Bw. Vura, aliyeshikwa tai alimzaba kofi.

Kijana alimwangalia mzee aliyekuwa nyuma yake kisha akamwachilia polepole, pale ambapo alikuwa ameketi, Bw. Siga alishusha pumzi.

"Sumba, tuondoke," mzee alimvuta mjukuu wake akiwa tayari kuondoka.

"Mnakuja kunivamia mpaka ofisini mwangu, mtajua mimi ni nani."

Yule mvulana alimwangalia tena Bw. Vura kwa macho ya uhasama kisha akaondoka, alikuwa mvulana wa kama miaka ishirini na nne hivi.

"Babu, ungeniacha niyafunze adabu haya masimbi," Sumba alimwambia babu yake.

"Mjukuu wangu, sikutaka ujiingize pabaya, ana ushawishi katika afisi kuu na sikutaka kukupoteza."

"Kwa nini samaki wakubwa kuwanyanyasa wadogo?!" Sumba alijiuliza akitikisa kichwa.

Waliondoka polepole, wafanyakazi waliacha kazi zao wakaanza kuwaangalia kama picha, Sumba alikuwa anatamani babuye amuruhusu arudi nyuma akamilishe alichotaka lakini hakufaulu.

Yule mzee mvi zilikuwa zimelanda kichwa kizima, lakini haikuwa bure. Alijua kwamba nchi yao Gunga ilikuwa nchi ya wachache ya walionavyo, nao wengine ambao hawana wakajifanya watumwa wa walionavyo wengine kwa hiari na kwa sababu ya hali ngumu.

Kule nyuma walikotoka, Bw. Vura alizua tena ugomvi kati yake na meneja wake. Siku hiyo aliiona kama iliyokuwa imempambazukia kuwa ya lawama kwa upande wake; kwanza, karibu amgonge bawabu wake pale langoni, kusudi la pili alivyoongeleshwa na Arina aliona chembechembe za dharau na mwishowe alikuwa amekabwa koo na mvulana ambaye hakujua asili wala fasili yake.

"Hao ndiyo wateja unaojishughulisha nao?!" Bw. Vura alimuuliza kwa hasira, "watu ambao hawana heshima wala hawajui utaratibu wa ofisini."

"Tulia boss, yashatokea."

"Unasema yashatokea sio! Au hata ulikula njama nao."

"Aka! Hata mimi mvulana huyo simtambui, lakini pole."

"Hilo nishakuonya kuniambia pole."

Bw. Siga alipokaa alipomwangalia tena mwenzake usonialitaka kucheka lakini akajizuia. Aliinuka akaelekea dirishani, kisha akafungua kupunguza joto la ofisini.

"Laizma atanitambua, yes," Bw. Vura alijiambia, "atajutia kunikaba koo."

"Usiyatie mo...,"Bw. Siga alisitishwa kwa kofi lililompata shavuni.

"Nisiyaweke moyoni, nambie basi niyaweke wapi!" Mwenzake alimuuliza akimshika tai.

"Hasira ni hasara," Bw. Siga alimshauri, "huenda ukafanya chochote cha ujinga na ukajutia maishani."

Bw. Vura alimwachilia polepole kisha akarudi kitini, alijua kilichomanishwa na mwenzake, hakutaka uovu uliokuwa ukienea mle ndani ujulikane kwa watu wa nje ya kampuni hiyo, pia hakutaka hakutaka mwenzake atibue kibuyu chake cha maziwa.

"Ulikuwa umekaa usifanye hata lolote kuniokoa kutoka kwa meno ya simba," Bw. Vura alimtania mwenzake akicheka, kicheko kilikuwa cha kumsahaulisha kuhusu yale ambayo alikuwa amemtenda.

"Ukianza kucheza ngoma, lazima umalize mwenyewe," mwenzake naye alimtania, "huwezi kuwasha moto kisha ukatarajia mwenzako kuuzima."

Bw. Vura aliinuka akachukua koti lake kisha akaanza kuondoka, naye mwenzake kuonyesha kwamba hakuwa na kisasi naye, akainuka kumsindikiza.

Bw. Siga hakuwa mtu wa kuonyesha hisia zake wazi usoni, lakini naye alikuwa amekasirishwa zaidi na kitendo cha mwenzake kumpiga kofi.

****

Labibu alipotoka shuleni alimkuta mamake amekaa mlangoni akapita pasi kuamba lolote, hali hii ilimshitua sana Bi. Tabasuri kwa sababu haikuwa kawaida yake.

"Labibu," Bi. Tabasuri alimuita baada ya dakika kadhaa, "njoo mwanangu."

"Naam mama," aliyeitwa aliitikia kutoka ndani.

Alitoka akaketi kando ya mamake, lakini akageuka na kuangalia upande mwingine. Mamake alimwangalia akitarajia ageuke wasemezane lakini Labibu akasalia vile vile.

"Labibu!" Mamake alimuita kwa mara nyingine, wakati huu sauti ilikuwa ya wasiwasi.

"Naam."

"Nini kinakutia majonzi?."

"Hakuna," Labibu alijibu akigeuka na kumwangalia kwa mara ya kwanza kutoka walipoanza mazungumzo, "hakuna lolote baya."

"Hapana mwanangu, nimekulea tangu utotoni mwako," mamake alimpinga, "mi' nakujua zaidi yako mwenyewe. Hi tabia umeanza lini mwanangu!"

Labibu alifikiri kumweleza Visa ambavyo vilikuwa vinazungumzwa juu yake shuleni mwao, lakini akahisi atakuwa anamuingezea maumivu.

"Mimi ni mamako mzazi, tena rafiki yako wa kwanza. Hebu nifungulie moyo wako uniambie kinachokuumiza."

"Umemuona baba tangu jana?!"

"Ndiyo, alikuja saa zake za kawaida na kuondoka alfajiri hata kabla ya jogoo wa kwanza kuwika."

Labibu alipomuuliza babake, mamake akajua bila shaka Kuna jambo ambalo bintiye alitaka kuzungumza naye, akafikiri labda ni kuhusu siku hiyo ambayo walikuwa katika boma la Bw. Mhifadhi na Bi. Alizeti.

"Kwa nini usiniambie mwanangu," Bi. Tabasuri alimsihi mwanawe, "sitamwambia yeyote."

"Nimetumwa nimuite baba," Labibu alimwambia nia a mjo wake.

"Kuna nini tena?!"

"Hakuna...eeh...," Labibu alikata maneno yake, "sifahamu wanalomuitia, mimi nimetumwa na mwalimu mkuu."

"Usiwe umezua zogo huko shuleni," mamake alimuonya.

"Sijafanya chochote mama," alijitetea, "mbona kunifikiria vibaya."

"Si hivyo mwanangu, namuogopa ba...," alikata maneno yake aliposikia mlio wa honi langoni.

"Amewasili!"

Bi. Tabasuri aliinuka akaenda kufungua lango, alikuwa akizongwa na mawazo kuhusu ambalo bintiye amefanya mpaka kutumwa nyumbani. Labibu alipokuwa ameachwa na mamake hakuwa na amani, alijua labda hata angemweleza mamake sababu ya mjo wake hangeamini.

Alitikisa kichwa na kufuta chozi lililokuwa limemtoka alipokumbuka yote ambayo yalikuwa yakisemwa juu yake shuleni kote Mkanya.

"I don't believe this," alijiambia kwa sauti ya masikitiko, "they say am like a weed in a flower garden, so they have to uproot me earlier so that I don't affect other students."

Bw. Nadama aliingia polepole kwa gari lake baada ya kufunguliwa lango na mkewe, kisha akaliegeza ndani ya kijumba cha mabati kilichojengwa kando ya lango hilo. Ulikuwa mwendo wa saa tisa za jioni alipofika nyumbani kwake kutoka kazini, alishuka na kuanza kuelekea mlangoni, alipomuona bintiye, kwa ghafla alikasirika.

"Umerudi tena," alianza akisonga kwa utaratibu, "umefika hata bila taarifa!"

"Ah! Mume wangu, hiyo si njia nzuri ya kukaribisha wageni," mkewe aliingilia kati, "unafaa kumjulia hali kabla ya chochote, hujui alikotokea kuko vipi!"

"Namuona yuko salama kabisa, hapana haja ya kumsalimu tena, au nimekosea."

"Unamuona yuko salama, lakini hujui nafsi na fikra zake au humuoni alivyo. Anaonekana mtu aliyekereka."

"Lazima aonekane msononefu kwa sababu anajua yale ambayo amefanya shuleni."

"Kwa nini unapenda kumuingilia na kumuwazia mabaya!"

"Kwani ana dirisha au mlango ndo nimuingilie, huku kumtetea kwako ndiko kunamfanya avimbe kichwa."

"Si kumtetea bali huo ndiyo ukweli, huwezi kumsingizia kitu ambacho hajafanya."

Pale alipokuwa ameketi aliinua kichwa alichokuwa ameinamisha kama kanga wakati wa mvua tangu majibizano kati ya wazazi wake yalipoanza akamwangalia babake, alishindwa kumuelewa kabisa, hata yale maongezi kwake aliyaona kama ya mzazi ambaye ameshindwa kutunza familia yake.

Babake pale alipokuwa amesimama alimwangalia lakini macho yake akaelekeza kando.

"Unaona tabia zake, anaangalia chinichini kama kondo," alimrudia mkewe, "utundu na utukutu wake unaweza kuona kwa tabia zake, 'mi nilisoma saikolojia, hawezi kunidanganya."

"Saikolojia ukasomea wapi!" Mkewe alimuuliza katikati ya kicheko, "utadanganya asiyekujua."

"Unaona tabia zako, unaleta mchezo wakati usiofaa, tabia zenu zinafanana, mama kama binti na binti kama mama."

"Unakosea mume wangu."

"Nakuwmbia ukweli, mtu akiwa na wake wawili kama wewe na watoto sita kama hawa, he is completely finished."

"Na mke akiwa na gumegume kama wewe, hana bahati maishani."

"Baba, naomba nikuulize swali," kwa mara ya kwanza Labibu aliyekuwa amekaa kimya alimuomba babake.

"Uliza, bora lisiwe la kishenzi."

"Maisha ni nini?."

"Unaona maswali anayouliza," Bw. Nadama alimgeukia tena mkewe, "maswali ya upuzi na ushenzi kama yeye mwenyewe."

"Ok Mr. Professor," mkewe alimrudishia baada ya kusikia matusi aliyomumiminia mwanawe, "ulisoma ukafika wapi! Ulaya, Marekani, Uholanzi au India. Nakuona uko papa hapa na rangi yako ni ile ile, ndo umuite mwanangu mpuzi."

Bw. Nadama alinyamaza baada ya kumuuliza swali lile, alishindwa hata madharau yalikotokea.

"Amekweleza sababu mjo wake?," alimuuliza tena mkewe.

"Hapana."

"Kama hajakwambia, m'mekuwa mkizungumzia nini?!"

"Alisema anataka kukwambia mwenyewe, mimi singefosi wakati anataka kuongea na babake."

"Basi niambie habuba wangu," Bw. Nadama alimwambia mwanambee wake kwa sauti ya upole, "lakini kama umekosa au umeghairi amri huko shuleni, nitakutifuatifua."

"Wee...! Usimletee mwanangu za kwako," Bi. Tabasuri aliingilia kati yao kuzuia mumewe kumpiga Labibu.

"Nilitumwa nije nikuarifu kwamba kesho tuandamane nawe mpaka shuleni," Labibu alimtolea sababu ya mjo wake.

"Kwa nini hawakusema mamako ndiye ambaye mnafanana kiakili."

"Tena unapingana na amri kutoka shuleni, lazima pana sababu murwa."

Baada ya kupingana pale kwa dakika kadhaa, alisalimu amri akaamua kuandamana na mwanawe kwenda shuleni.

Walianza kupiga gumzo ya kifamilia na utofauti uliokuwepo wakatupa mbali na kupiga gumzo ya furaha. Hata pale walipokaa, Labibu alikuwa akiwazia kitu ambacho kingetokea wakati babake angejua ukweli.

Bw. Nadama naye mtima ulikuwa ukimwenda mbio, hakujua fumbo ambalo angefumbuliwa shuleni lingekuwa la furaha au huzuni, naye Bi. Tabasuri alikuwa akifikiri kumhusu mwanawe na yale ambayo alikuwa amebeba moyoni.