SURA YA TANO

Mwendo wa saa mbili asubuhi, Bw. Nadama na bintiye waliondoka baada ya kupata staftahi ya chai kwa mayai.

Labibu hakula chochote kwa sababu ya kukosa hamu kwa kile kilichoandaliwa na pia kwa sababu ya yaliyomsumbua akilini. Safari iliendelea bila maongezi mle ndani kati ya baba na mwana.

"Mwanangu, hebu niambie sababu ya kuja kwako nyumbani?" Babake alimuuliza baada ya kusafiri kwa muda mrefu bila mazungumzo kati yao.

"Mimi sijui kilichofanya," Labibu alimficha babake, "mie niliitwa tu na mwalimu mkuu akaniambia nije nikuite."

"Hebu fikiri, muhula uliopita hukufanya kosa lolote au kumtenda mwenzako karaha!"

"Hakuna, sijafanya lolote baya."

"Au ulikaidi amri ya mwalimu?."

"Hapana."

"Basi kwa nini ukatumwa nyumbani," babake alimfokea, "ulitumwa pasipo na kosa lolote! Hapana...nikijua ulichofanya, utajua kucha zangu nilizoficha kwa watoto watundu kama wewe."

Labibu alikuwa amejibana mlangoni kuondokea kidole cha babake kilichokaribia usoni, alijua hata akimweleza ukweli atazidi kukata kwa sababu ya kiburi kilichokuwa kichwani.

Alijua kwamba yale ambaye yalikuwa yakimtendekea babake alifahamu lakini akakata kuamini ukweli uliodhihirika wazi.

"Dad, nilikuuliza swali," alimuanza tena babake baada ya kimya cha muda.

"Swali lipi?."

"Nilikuuliza unavyoweza kufananisha au kufafanua maisha."

"Mi' sijui," babake alimjibu akionekana aliyeudhika, "we ambaye umeishi sana na kuona mengi hebu nambie."

"Maisha ni kama kusafiri katikati ya msitu wenye wanyama na adui zako kwa pamoja, utapitia mengi ya kuogofya na uchungu. Ukifika upande wa pili salama na kuwaambia wenzako uliyopitia hawatatuamini, wengine watafikiri ni kutaka sifa. Licha ya hayo yote wanaojua ambayo umepitia ni wawili tu; ni Maulana na nafsi yako, hao ndio ambao watakuwa mashahidi wako wakuu. Kitu kingine kigumu kufanya hapa duniani ni kuidanganya nafsi yako. Unaweza ukafanya vyote ukafaulu bila tashwishi yoyote isipokuwa kujidanganya," Labibu alimumwagia babake yaliyokuwa moyoni mwake.

"Asante kwa maneno yako ya staha na hekima changa," babake alimdunisha.

Waliendelea na safari wakiwa kimya hadi wakafika mbele ya lango la shule yake, Bw. Nadama alipoangalia saa yake, alikunja sura kama mtu aliyekunywa maji ya mshubiri. Aliona ni kama uharibifu wa raslimali yake, aliona anapoteza wakati kwa kitu ambacho hakitamfaidi kwa njia yoyote. Walisimama langoni kwa dakika ishirini kabla mlinzi hajafika.

"Tafadhali tufungulie," Labibu alimuomba yule bawabu, "tunasubiriwa na mwalimu mkuu."

"Ah!," yule mlinzi alishtuka alipomuona Labibu, "ni huyu msichana wa mazingaobwe!"

Bw. Nadama alimwangalia mwanawe kwa jicho ambalo kanakwamba liliuliza "msichana wa mazingaobwe ni yupi?."

Maneno ya yule mlinzi yalifanya Labibu akaanza kulengwalengwa na machozi, alikuwa ashapata jina la kumdunisha katika jamii nzima ya shule yao. Kwa haraka bawabu alifungua akawapisha na kufunga lango nyuma yao.

Wanafunzi waliokuwa nje nyanjani wakinadhifu shule yao, walimwangalia Labibu kwa macho ya kuogopa.

"Mbona wanakuangalia hasa wanakuogopa?!" Babake alimuuliza akiegesha gari kivulini.

"Mimi sijui."

"Hujui, wakati umefika ambao yote ambayo umekuwa ukifanya yatafichuka."

Wakiwa bado wanaongea mle ndani ya gari, mwalimu mmoja alifika na kusimama kando yao. Bw. Nadama alipomwangalia usoni aliona alama za kucha, alifika na kusimama kama sanamu. Kununa kwake kulikuwa idhibati kamili kwa Bw. Nadama kuwa mambo hayakuwa mazuri.

Labibu alimwangalia kwa uoga, akafungua mlango polepole na kushuka.

"Hata ushachelewa," yule mwalimu alimwambia kwa hasira, "uliagizwa kufika hapa saa moja unusu."

"Safari ndo ndefu."

"Safari ilikuwa ndefu, kwa nini hukuwahi mapema ndo uje utoe sababu ambazo hazina kichwa na miguu."

"Naomba radhi," Labibu alimuomba msamaha kwa unyenyekevu.

"Mwenyewe utamweleza mwalimu m..."

"Samahani mwalimu," Bw. Nadama aliyekuwa amesimama kando akiwasikiliza alimkatiza, "naona ingekuwa heri tufahamiane kabla mambo mengine hayajafuata."

"Tufahamiane! Tufahamiane! Naona huo ndio msamiati wa pekee ulioshika kutoka shuleni, mjuane na nani!" Yule mwalimu alimjibu kwa sauti ya kutisha mpaka Bw. Nadama akasonga nyuma hatua moja, "let me hope you are not like your daughter."

Waliandamana wote watatu kuelekea katika ofisi ya mwalimu mkuu. Mwalimu na Bw. Nadama walikuwa mbele kisha Labibu akawafuata nyuma unyounyo, moyoni alitamani wasimpate mwalimu ofisini au shughuli ya ghafla itokee.

Walipofika mlangoni, mwalimu alibisha.

"Karibuni," sauti nzito iliwakaribisha kutoka ndani.

Walipofungua mlango na kuingia ndani, Labibu alishtuka. Alikuwa ametarajia kumpata mwalimu mkuu pekee yake au na walimu wengine wawili hivi lakini akapata staff nzima imemngojea. Bw. Nadama alipokuwa analisha macho yake mle ndani, kitu kimoja tu ndicho kilifanya awe na hofu, sura za kutisha ambazo wale walimu wote walikuwa wamevalia na kumkazia mwanawe macho.

"Have a seat," mwalimu mkuu aliwakaribisha.

Alivuta kiti kwa utaratibu akaketi, Labibu alikuwa anahisi baridi, "upepo baridi umevuma juu ya kondoo mchanga aliyenyolewa mafuma" aliwazia, alinyosha mkono wake polepole kuchukua kiti lakini kikaondolewa na mwalimu mmoja, kitendo kile kilimkasirisha sana Bw. Nadama lakini akajituliza.

"Alikwambia sababu iliyofanya tukamtuma nyumbani?," Mwalimu mkuu alimuuliza Bw. Nadama.

"Hakuniambia chochote."

"Hata mwenyewe nitakwambia sasa hivi, lakini najua hutaamini, utafikiri tunakuchezea," mwalimu alianza kumweleza, "hata hawa walimu hizi si sura zao za kawaida, ni kwa sababu ya vijimambo ambavyo mwanao amewatenda."

Bw. Nadama alimwangalia mwanawe pale pembeni alipokuwa amesimama akaona machozi yanamtoka, mwalimu aliyefika kuwapokea walipowasili alikuwa akimwangalia Labibu kwa macho ya kuchukiza.

"Angalia alivyomtenda mwalimu wangu," mwalimu mkuu aliendelea akimwashiria mwalimu aliyejeruhiwa usoni kwa kidole, "hebu njoo utueleze mwenyewe."

"Ulikuwa mwendo wa saa nane aliponitenda unyama huu," yule mwalimu alianza kusimulia kwa hasira, "mimi ndiye mwalimu wake wa darasa, nilipokuwa nafunza somo la Biolojia alionekana mtu ambaye fikra zake hazikuwa darasani. Alikuwa ameangalia nje ya dirisha kama mtu ambaye alikuwa anaangalia kitu fulani, nilipoenda karibu yake kuangalia alichokazia macho, sikuona chochote ndipo nikampiga kofi kumrudisha darasani, hapo ndipo kizaazaa kilipotokea; alinivamia akaanza kunipiga kama gunia la maharagwe, kama si mwalimu mwenzangu kuja kuniokoa, sijui kama ningekuwa hapa kwa sasa."

"Kuna mwalimu mwingine yeyote ambaye alikuwa asharipoti kisanga kama hicho kwako kabla ya hayo?!"

"Ndiyo, lakini sikuamini. Nilikuwa nishapata ripoti nyingi kuhusu hii tabia lakini nikapuuza."

"Sasa wewe kama mzazi unasema nini?," mwalimu mkuu alimtupia babake Labibu swali, "kwa sababu hatuwezi kuacha mwanafunzi mmoja aharibu shule, kumbuka samaki mmoja harabu ya nzima."

Bw. Nadama alishindwa hata la kumwambia aliyemuuliza swali, akili yake ilikuwa imesimama kufanya kazi, walimu walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine mpaka wakaisha mle ofisini, mwalimu mkuu na Bw. Nadama, wote wakageuka na kumwangalia Labibu.

***

Bw. Siga alimwangalia tena Arina pale alipokuwa ameketi akashindwa kilichokuwa kinamliza, walikuwa wamekaa mle ndani kwa nusu saa pasipo na mazungumzo. Tangu Arina alipoingia saa mbili za asubuhi mpaka saa mbili na nusu, hakuwa amesema lolote isipokuwa lugha ya machozi.

"Arina!" Mwenzake alimuita.

Aliyeitwa hakuitika, mwenzake akanyosha mkono kumgusa lakini akasitisha. Alijaribu kuvuta kumbukumbu zake akumbuke popote alipomuasi lakini akashindwa.

"Ongea nami tafadhali," Bw. Siga alimuomba, "nitajua vipi kinachokuliza usipozungumza!"

Arina aliinua kichwa chake taratibu na kumwangalia Bw. Siga, macho yalikuwa mekundu. Bw. Siga aliogopa akarudi kitini baada ya kuonana naye macho kwa macho. Arina alikuwa ameshindwa kilichomketa.

"Kama nimekukosea naomba unisamehe," Bw. Siga aliomba radhi, "kwa sababu ni kama hutaki kuzungumza nami."

"He almost raped me," Arina alimwambia kile alichokuwa amefungia moyoni katikati ya kilio.

"Who?!" Bw. Siga alimuuliza kwa mshangao.

Arina alitokwa na machozi na kamasi kwa pamoja, akapenga kamasi iliyokuwa inamteremka mdomoni kwa kitambaa. Alijua mwenzake hatayaamini maneno yake akimwambia mtu aliyetaka kumbaka. Yale maneno yalifanya Bw. Siga akaanza kuumwa na kichwa.

"Nieleze kwa haraka, hilo si jambo la mchezo," alimwambia kwa msisitizo, "hebu niambie haraka nione nitachukua hatua ipi, hayo usemayo si ya mzaha."

"Ni mkubwa wako," Arina alimwambia akijaribu kuficha jina halisi la mdhulumu wake.

"Hebu kuwa wazi. Mimi nina wakubwa wengi; Bw. Vura, wateja wangu na hata nyie pia ni wakubwa wangu hapa kazini."

"Ni Bw. Vura," Arina alimwambia kwa sauti ya masikitiko.

Bwana Siga alibaki kinywa wazi baada ya jina kutajwa, Arina baada ya kumtaja machozi yalianza kumtoka.

Alifuta machozi na kumwangalia aliyekuwa mbele yake kwa macho ya kuomba msaada. Alikuwa amefika pale ofisini akiwa na matumini ya kupata usaidizi kutoka kwa mkubwa wao.

"Hebu rudia tena," Bw. Siga alimwambia baada ya kimya cha sekunde kadha.

"Ni Bw. Vura."

"Una hakika na yale usemayo?!" Bw. Siga alimuuliza akionyesha kichwa chake kwa kidole cha shahada, "au umepagawa!"

"Ni kweli, mimi siwezi kupanga maneno kama hayo," Arina alimjibu kwa upole, "au ukiniangalia ni kama nimepagawa!"

"Akiwa hapa unaweza kurudia maneno yako?."

"Ndiyo, nitarudia neno baada ya jingine kwa sababu nimekweleza ukweli."

Bw. Siga alinyamaza tena na kumwangalia Arina alipokuwa, hata naye moyoni alijua lazima aliyoambiwa yalikuwa ya kweli lakini aliogopa kumkabili Bw. Vura.

Maswali aliyokuwa anamuuliza alitaka mwenzake kuacha kilichokuwa kimemtendekea.

"Hebu nieleze kisa hicho kikivyotendeka."

"Ilikuwa siku ya Jumapili wiki jana kilipotokea," Arina alianza kusimulia.

"Endelea."

"Alifika katika wadi tulikokuwa tukimuuguza babu."

"Alianza kuugua lini? Na kwa nini hukunijuza kwamba Kuna mgonjwa!"

"Si babu wangu wa uko, bali kwa sababu ya heshima tu. Ni mmoja wapo wa wafanyakazi hapa ndani."

Bw. Siga aliangalia chini kwa haya baada ya kujiona kama anayepuuza maslahi ya wafanyakazi wake, Arina naye kwa upande mwingine alimuona mtu asiyewajibika.

"Hukujua kwamba Bw. Rufai ni mgonjwa?," Arina alijikuta akimuuliza.

"Ningejua namna gani bila yenu kunipa taarifa," alijitetea, "endelea."

"Naona hamtujali kabisa, tunaishi humu ndani kama wanyama porini ambapo mmoja hamjali mwenzake. Hata heri wanyama wanajua kutunza vikembe vyao, hapa bora nyie muone kazi inaendelea, hamtaki kujua hali zetu, tunachokula, tunachovaa na hata usalama wetu."

"Hayo tena yametokea wapi!"

"Si mambo ya kutokea, kama huwezi ukajua kama mmoja wetu ni mgonjwa, hilo linamaanisha hatuna manufaa kwenu, kwa sababu tungekuwa na manufaa mngetujali zaidi."

Bw. Siga alijikuta amezuba kwa Arina kwa sababu ya yale maneno, alijua ni kweli lakini mapuuza yenyewe yalitoka kileleni mwa mti.

Mwenyewe alijua aliyokuwa anapitia akijaribu kuwatetea alipoajiriwa na Bw. Vura. Alijaribu kwa hali na mali kuweka mambo sawa lakini ikawa kama sikio la kufa lisilosikia dawa.

"Nishakusikia, hayo tutashughulikia," alimpa imani, "lakini kwanza niambie kilichotokea."

"Tulikaa naye hospitalini mpaka usiku, wauguzi walipoleta bili ya mgonjwa ilikuwa shilingi elfu nane...," alikatizwa na chozi lililomdondoka mdomoni.

"Usilie, machozi si mraba utakaofuta yaliyotokea."

"Alitoa shilingi mia mbili pekee," Arina alimwambia akitikisa kichwa, "mpaka sasa babu hajakamilisha matibabu yake kwa sababu wauguzi wote walikula yamini kutomhudumia tena mpaka peni ya mwisho itolewe."

"Ufedhuli mkubwa huo!"

"Saa tatu kasorobo aliniagiza niende kuangalia chumba cha kulala, nilikataa lakini akanisisitizia. Baada ya kuzunguka kwa saa nzima, nilipata chumba katika jumba la wastahiwa la Mbalakwe kisha nikampigia simu na kuondoka."

"Kama uliondoka, ikawaje tena akajaribu kukunajisi."

"Nikipokuwa naondoka tulikutana kwenye mapokezi akaniagiza niende kukagua chumba alichopewa. Nilipanda vidato kwenda kukichunguza, lakini nilipokuwa nafanya alivyoniagiza, nilishtukia amesimama mlangoni. Sura 'kaikunja kama tomoko, mara moja alinifi...," Arina alikatiza maneno yake.

"Why didn't you report earlier?."

"Niliripoti kwa wakuu wa jumba hilo, lakini mpaka sasa sijaona kama wamechukua hatua yoyote ndo imenilazimu nije nitafute msaada wako."

"Kando nami, umemweleza mwingine yeyote?."

"Hapana mtu mwingine."

"Hilo ulifanya jambo zuri kwa sababu ungekuwa umeharibu picha kati ya wenzako."

Bw. Siga hakumwambia haya kwa sababu ya kumjali, bali alitaka kuficha tabia mbovu za mdosi wake, alitaka aliyoambiwa yabaki gizani yasitoe hata ukucha wake katika mwanga kwa sababu ukucha ungeonekana watu wangetia bidii za mchwa waone kiwiliwili kizima.

"Ukifika mbele ya hakimu unaweza kusema yale ambayo umeniambia?," Bw. Siga alimuuliza, "usiwe unapalia makaa pasipofaa."

"Nitasema.

****

Labibu alifika ofisini mwa Bw. Haima moyo ukidunda kwa nguvu kama ulotaka kutoroka, alipofika mlangoni mtu wa kwanza kumuona alikuwa Bw. Hajiri, mwalimu wake wa Biolojia na pia msimamizi wa muungano wa wakristo shuleni humo.

Alipoangalia mbele yake alimuona Bw. Haima lakini mtazamo alopewa ukafanya akaingiza baridi na kusita kuingia.

"Ingia haraka," Bw. Haima alimharakisha alipoona amesimama mlangoni, "sina wakati wa kupoteza."

Kwa haraka Labibu aliingia akitetemeka mbele ya walimu wake, Bw. Hajiri alimwangalia kwa huruma, alijua hatua ambayo mwalimu mkuu atachukua wakati huu haitakuwa nzuri kama mwanzo.

"Yako yamekifika kooni, na kwa sasa yananisakama," mwalimu mkuu alianza kwa sauti ya chini lakini ya hasira, "nahofia kwa sababu uamuzi wangu mara hii utaona nankudhulumu, ila sina budi."

"But sir... what have I done?!" Labibu alimuuliza akitoka alipoketi na kupiga magoti.

"Hujui ulichofanya, usinichukue kama mtoto mdogo," Bw. Haima akimkemea, "kila utendalo shuleni humu nalijua, macho yangu yanaangaza kote hapa shuleni na maskio yangu yana nguvu za kusikiza ndoto zako."

"Acha nikifafanulie kitu mwa..."

"Hapana bwana mtetezi," mwalimu mkuu alimkatiza mwenzake, "najua unataka kumtetea, lakini leo sidhani kama utafaulu. Nawe Jumatano saa tano za usiku ulikuwa wapi?."

Labibu alipokuwa amepiga magoti alimwangalia mwalimu mkuu kwa mshangao, akajionyesha kifuani kwa kidole, naye mwalimu akaitikia kwa kichwa.

Alijaribu kukumbuka alipokuwa masaa yaliyotajwa na mwalimu bila mafanikio, alichokumbuka ni alivyosalia darasani baada ya wenzake kuondoka saa tatu, alikumbuka akivyoanza kudurusu vitabu vyake. Hayo ndiyo yaliyompitia akilini.

"Nilikuwa bweni nikilala," aliamua kumdanganya baada ya kushindwa kukumbuka kilichotokea.

"Umeamua kunidanganya kabisa!" Mwalimu mkuu alimwambia katikati ya kicheko cha kuudhika, kisha kwa ghafla akabadili sura, "were not seen seeting in basketball square doing some mysterious symbols in the air, nimekukumbusha ulipokuwa."

"Mimi..."

"Ndiyo, tena ulitaka awe nani mwengine."

"Yaliyosemwa na mwalimu mkuu ni ukweli," Bw. Hajiri alichangia, "lakini naomba unisikilize mwalimu wangu, kwa muda wa miezi mitatu sasa nimekuwa nikimchunguza Labibu kwa makini nikagundua kwamba, wakati mwingine huwa kama mtu asiyejielewa, wakati huo ndio ambao huwa anafanya vioja unavyozungumzia."

Labibu alimwangalia mwalimu wake kama mtu asiyeamini, alitarajia mwalimu amtetee mbele ya mwalimu mkuu lakini haikufanyika.

Alijua uhusiano wake na shule ya Mkanya aliyoipenda kwa dhati ushakatika na yule wa kuunganisha alikuwa ashajitoa akamuacha pabaya. Machozi yalimtoka, akamwangalia mwalimu mkuu.

"Lakini tungempa wakati tuchunguze chanzo cha tabia hii," Bw. Hajiri alimuomba mwalimu mkuu.

"Nilijua utafikia kumtetea," Bw. Haima alimkaripia mdogo wake, "ombi lako limekataliwa, huyu mwanafunzi amekuwa msumbufu. Jina lake limekuwa wimbo kwa midomo ya walimu na wanafunzi kwa jumla. Vituko vyake vimejaa chungu hadi vikaanza kububujika na kuzagaa sakafuni kote."

"Kumtaliki au kumtuma nyumbani si suluhisho, kumbuka pia ni miongoni mwa wanafunzi bora shuleni humu."

"Kama ubora wake ndiyo unaompa kiburi, basi na hatuutaki tena. Nawe unanishangaza hata zaidi, kati ya walimu wangu hamsini wewe ndiye unayemtetea."

"Ni kwa sababu najua ubora wake, wao wanajua tu ubaya na hata wengine hawamfahamu, ni fununu wanazosikia," Bw. Hajiri aliendelea kumtetea mwanafunzi wake, "maziwa yanabaki na uzuri wake, usione yamebadilika rangi au yameharibika ukafikiri hayana manufaa kwa mhifadhi wake."

Bw. Hajiri alimwangalia Labibu alipokuwa amepiga magoti akamhurumia, alijaribu kwa kila namna kutomtenganisha na shule yake bila mafanikio. Kila sababu aliyotoa kumsaidia, mwalimu mkuu alipata nyingine ya kumpinga.

Bw. Haima alimwangalia Labibu kwa macho ya utulivu.

"Hata nilimpigia babake simu aje tuzungumze maneno yake, lakini akaghairi wito wetu."

"Labda alikuwa nje ya mji au kwa biashara zake nje ya nchi," Labibu alimtetea babake.

"Basi anaona biashara zake ni muhimu kuliko maisha yako, nasi tumeona heri uende ukae nae."

"Usifanye hivyo tafadhali," Labibu alimlilia mwalimu mkuu.

"Eeeh... tafadhali mr. Haima, tumhifadhi hapa shuleni tukifanya uchunguzi," Bw. Hajiri alijaribu kumtetea kwa mara nyingine, "pengine yale yote ambayo ushasikia ni umbea mtupu."

"Umenichosha kwa maneno yako," mwalimu mkuu alimkemea, "nitajua vipi utakayoniambia baada ya uchunguzi yatakuwa ya kweli. Kila neno litokapo katika kinywa cha msemaji, mwenyewe husema ni kweli, hakuna siku atakiri kwamba ametamka uongo wala maneno yatokapo kinywani huwa hawajandika juu yake kama ni uongo ama ukweli."

"Lakini mia..."

"Fyata ulimi wako, niongeapo sitarajii uwe unaongea. Kama unaona ni vigumu kufanya kazi chini yangu, basi kafungue shule lako uendeshe mambo utakavyo. Hapa kitu kitakapotokea, mie nitaulizwa na si wewe, na kwa sababu hiyo sitaki uingilie uamuzi wangu."

Bw. Haima alikuwa ashakasirika kwa sababu ya kupingana, Labibu pale alipokuwa alikuwa amelia mpaka machozi yakamkaukia kifuani.

Bw. Haima alimuamuru Bw. Hajiri aende amwambie mlinda saa kupiga kengele baada ya kukata kauli yake, aliyetumwa alitoka ingawa shingo upande.

Mle ofisini Labibu alimwangalia mwalimu mkuu kwa macho ya kuomba hisani, lakini akiyeangaliwa akainuka na kumuondokea. Pale aliposimama aliona angepoteza kazi yake iwapo wakuu wake wangeingia shuleni humo na kupata msukosuko uliokuwepo.

"Lakini mwalimu nisamehe, sitarudia tena," Labibu alimuomba msamaha akimuangukia miguuni, "adabu hiyo ni kama kaa la moto mgongoni mwangu, siwezi kuvumilia."

"Neno msamaha limekuwa kama wimbo mdomoni mwako. Ni mara ngapi nishakusamehe lakini ukarudia. Hata ukimsafisha nguruwe namna gani na kumpaka manukato ya kila aina, lazima atarudi matopeni," Bw. Haima alizidi kumkazia kamba, "nimechoshwa na vituko vyako, jaribu kwingine."

Labibu alishindwa maneno ambayo atatumia kubadili uamuzi wa mwalimu ili asimtaliki, aliinuka alipopiga magoti akaketi.

***

Bi. Tabasuri alimngoja mumewe sebuleni, aliketi karibu na mlango akiwa na nia ya kumuamkua apitapo kabla hajanzisha mazungumzo.

Bw. Nadama alitoka chumbani mwao kwa haraka akitengeneza tai yake, alipofika mlangoni akamuona mkewe alisitisha mwendo akaingia ndani.

"Kwa nini haraka hivi mume wangu?," Alimuuliza akisimama mlangoni kumzuia asitoke, "au hujui haraka siku zote haina baraka!"

"Hivyo ndivyo ujidanganyavuo!"

"Kutoka ulipotoka shuleni, hujazungumzia chochote juu yake."

Mumewe alimwangalia kwa macho ya kumkashifu, akajibana ubavuni apate nafasi ya kupenya nje lakini akashindwa. Polepole akirudi na kujitupa kochini kisha mkewe akatoka mlangoni na kwenda kukaa kando yake.

"Kwa nini hutaki kuzungumzia chochote kuhusu ziara yako shuleni anakosomea mwanetu?!" Bi. Tabasuri alianza.

"Usiniulize swali jingine la aina hiyo, au," Bw. Nadama alimtishia akisimama, "utajionea."

"Wengi washajionea cha mtema kuni, nilifikiri nitajionea cha mkata chuma!"

"Unaona, akili zenu zinafanana tu, nyote ni kama mliumbwa na bongo zilizolala."

"Hata kama tuliumbwa kwa zilizokufa, ni lazima nijue kuhusu mwanagu, chako kikioza hakikunukii."

Bw. Nadama alisimama katikati ya sebule, kumbukizi za yale matukio tangu walipofika kwenye lango la shule zilimrudia, hakutaka kumwambia chochote kuhusu aliyokuwa amesikia na kujionea kwa sababu alijua atamtia majonzi.

Aliangalia saa yake ya mkononi kisha akarudi kochini tayari kumsimulia aliyokuwa ameambiwa na Bw. Haima.

"Nafikiri mwanao hivi karibuni atakuwa mwendawazimu," Bw. Nadama alimwambia kwa sauti ya chini.

"Unaezaje kusema hivyo kuhusu mwanao," mkewe alimkaripia, "you don't care..."

"When you care too much for someone she becomes careless."

"Sasa hiyo ndiyo sababu hutaki kumjali!"

"Haswa, ungekuwa pale shuleni ungefedheheka kabisa, vituko vyake amevitoa nyumbani mpaka shuleni, tena ashavuka mipaka mpaka kwa walimu."

Bi. Tabasuri alimsikiliza, mumewe alianza kuelezea tukio baasa ya jingine jinsi alikuwa amesimuliwa. Picha ya yule mwalimu aliyekuwa amejeruhiwa na mwana wao ilimjia.

"Kucha zikizomkwaruza zikikuwa kama za paka lakini wao wenyewe wanasema ni Labibu."

"Nawe hukufanya chochote kumtetea, uliyaamini yote uliyoambiwa kama mjinga."

"Ningefanya nini? Kama kutokea langoni ushahidi ulianza kujitokeza wenyewe, wenzake walimwangalia kwa uoga mpaka nikafiri nimetembea na zimwi garini."

"Ah! Mwanangu kindakindaki, alikuwa vipi katikati ya meno ya simba," mkewe alikuwa ashaanza kutokwa na machozi, "hata hungeweza kusema lolote uonekane mzazi anayewajibika."

"Unazungumzia kuwajibika, sikupewa hata nukta ya kusema lolote na hata ningepewa singeweza kusema lolote. Kama walimu wake wenyewe walimwangalia kwa macho mabaya kama ambao wangemrukia wakati wowote na kumtafuna angali hai."

"Naona sasa sababu yako ya kukataa wito wao! We ni mzazi wa aina gani, hujui hatua watakayochukua baada ya kughairi wito."

"Wewe si kiwete, ungeabiri gari uende ujionee tope ambalo ungepakwa na mwanao, siwezi nikarudi huko hata kumwanagal..."