Labibu aliondoka chumbani mwake akaelekea barazani angalau kupumuzika, hakuenda kula soga na mamake ilivyokuwa desturi yake ya wakati kama huo. Mamake kwenye veranda alipokuwa ameketi akifuma kitambaa alikuwa akimtupia jicho mara kwa mara.
"Tena Kuna tatizo lipi?!" Mamake alijiuliza akiinuka alipokuwa, "alionekana mzoefu, lakini tena!"
Alianza kuelekea alikokuwa bintiye, alipofika karibu yake ndipo alipotambua kwamba mezani palikuwa na kijikaratasi.
Labibu alipoona mamake anamjia, alijkunjakunja karatasi lililokuwa mbele yake likawa duara dogo kisha akalitupa chini ya meza.
"Karibu mama," alimkaribisha akivuta meza kwa upande wake kumtafutia nafasi ya kupenya.
"Asante mwanangu," mamake alimshukuru akiketi, "kuna yeyote amekutenda maudhi!"
"Hapana, lakini kwa nini kuuliza?."
"Sijazoea kukuona ukiwa umekaa pekee yako, wala sipendi kabisa. Kama kuna yeyote amekukosea kati yangu na babako basi naomba msamaha."
"Hakuna yeyote, ningekwambia," Labibu alimwambia akimlalia begani, "nilikuwa napumuzika hapa nikidurusu siku zangu za shuleni."
"Ni vizuri kujikumbusha enzi zako za shule, lakini si mara kadha," mamake alimshauri, "ni kama kutamani tausi aliyekuponyoka mikononi akakimbilia msituni."
Bi. Tabasuri aliinuka akaondoka bila hata kumuarifu bintiye alikokuwa anaelekea, Labibu pale alipokuwa alimwangalia akatabasamu. Alianza kukumbuka maisha yake ya zama katika shule ya chekechea alivyokuwa akipewa na mamake viazi vitamu kwa uji ndani ya kipira kidogo kila asubuhi alipoenda shuleni.
Alipokuwa angali anasafiri katika zama yake, alimuona mamake akimjia akiwa amebeba nyuzi za rangi mbili kwa mkono mmoja; rangi nyekundu na rangi nyeusi, kisha mkono mwingine ukabeba kitambaa alichokuwa anafuma mwanzo.
"Leo utakuwa katika darasa la kufuma vitambaa," mamake alimwambia akiweka alivyobeba mezani.
"Kwa nini madarasa yako yasianze kesho," Labibu aliteta akisukuma kando uzi mweusi, "leo najihisi mchovu, sidhani kama kipindi chako nitang'ata chochote."
"Uvivu usikutawale, hebu tupilia mbali sifa hiyo," mamake alimuonya, "lazima mwanamke katika nyumba yako uwe mwenye bidii ili kuijenga au utaiboromosha."
"Nakuelewa mama, lakini leo sikuwa tayari kwa mafunzo yako."
"Ni lazima uwe mwenye bidii, au mwenzako atakuchukua na kukuendesha atakavyo akijua hutoenda popote. Hata bibi yangu aliniambia mwanamke hapati sifa kutoka kwa urembo au anavyovalia pekee, bali pia hutokana na kazi ambayo mikono yake imefanya."
"Anaonekana alikuwa mtu mwenye hekima," Labibu alimwambia mamake akichukua mmojawapo ya sindani zilizokuwa kwenye uzi mweusi.
"Ni kweli, alikuwa mtu wa kuheshimika katika jamii yake, nami hata nikaitwa kwa jina lake, basi vivyo hivyo lazima niwe kama yeye."
Labibu bila kuelekezwa na mamake, alianza kufuma kitambaa, alipofuma miviringo miwili na kukitazama, kilimchukiza. Kitambaa chake hakikuwa na umbo halisi, kilikuwa kimeshonwa kombo.
Mamake alipoangalia umbo la mfumi mwenzake alicheka, naye aliyechekelewa akachukua tena sindani kubahatisha, mara hii ya pili sindani ilimdunga kidole cha pete.
"Huwezi kufanya kitu vema ukiwa mwenye hasira," mamake alimshauri. Labibu alimwangalia mamake bila kutamka lolote kwa sekunde kadha.
"Mum..."
"Na'mbie mwanangu."
"Unafikiri kwamba kweli nitafanikiwa kurudi shule?!"
"Ndiyo mwanangu, kwa sasa babako kiguu hakibanduki njiani kwa sababu hiyo."
"Alikuwa na wakati wa kuweka mambo yangu laini lakini akauchezea," Labibu alimwambia mamake kwa masikitiko, "unga ukishatiwa chachu hauwezi ukarejea hali yake ya kawaida tena."
"Mbona unaniambia hivyo? Hata huna shukrani anavyopambana upate maisha mema."
Labibu hakumjibu tena mamake, aliinama chini ya meza akachukua kikaratasi alichokuwa amekunja na kuweka mikononi mwake. Bi. Tabasuri alimwangalia bintiye kwa mshangao kisha akakiangalia kile kikaratasi alichokuwa amekabidhiwa, kwa upole alikikunjua moyo ukidunda kwa nguvu.
Shule Ya Upili Ya Mkanya,
S.L.P 18700,
Mikumi.
27/5/2020.
Kwa Bw/Bi....
Kuh: Labibu
Ninapochukua kalamu yangu kuandika waraka huu akili zangu ziko razini kabisa, labda utakapoisoma utafikiri niliandika nikiwa nimepiga mtindi au kama nimepagawa. Wengine watadhani labda nina kisasi kwa sababu ya yale ambayo nitaandika.
Labibu amekuwa mwanafunzi wangu katika shule hii kwa miaka mitatu, huu mwaka wa nne ulipoanza, alibadilika kitabia kabisa hata asiweze kufuata amri anazopewa. Hapo awali alikuwa mwanafunzi mtiifu na msikivu kwa kila maonyo aliyopewa, lakini haya yote yalibadilika alipohitimu kuwa mkufunzi mwakani, sijui ni kiburi, utundu au nitaeleza kwa namna gani.
Namuomba mwalimu yeyote atakayepata barua hii asikubali asajiliwe katika shule yake, ni hatari kwa wanafunzi wengine wapenda amani. Tabia zake ni kama ugonjwa usio na tiba na ili kuepukana na maradhi yake ya tabia mbi, ni heri asikaribishwe popote. Sisi tulimchukua kama mwanga wa shule yetu, lakini baada ya kushindwa kumvumilia, tumeamua kumtema.
Najua wengine watanichukua kwa ubaya baada ya kusoma waraka huu, lakini yale ambayo nimeeleza ni ukweli mtupu. Nimeamua kuanika tabia zake peupe kuonekana kwa yeyote aliye na hekima, huyu mwanafunzi ni nusu dengu nusu donda. Nawe ukiwa mwalimu mkuu na unafikiri kumchukua jiulize; je! Mfupa ulomshinda fisi mbwa atauweza!
Wako Mwaminifu,
Haima Mkosi(mwalimu mkuu)
Baada ya kusoma barua aliyopewa, aliifumbata ilivyokuwa kisha akaitupa ilikokuwa imeokotwa, aliweka kitambaa alichokuwa anafuma kando kisha akamwangalia bintiye. Alimwangalia kwa macho ya upendo wa mzazi, Labibu naye alimwangalia kwa macho ya machozi.
"Hilo lisikutie hofu," mamake alimwambia.
"Sina hofu yoyote," Labibu alimwambia akijitia hamnazo, "mzazi anayejua uchungu wa mwana kufikia kiwango cha kumharibia mwana wa mwenzake maisha."
"Asiyekujua haku..."
"Lakini mimi amenijua kwa muda, miaka mitatu si nukta tatu."
Labibu alikuwa amemkatiza kwa hasira iliyomjia, "hawatujali kabisa" alifikiri. Alifuta machozi akaangua kicheko kwa ghafla kilichomshitua mamake.
"Tena kuna nini!" Mamake alimuuliza kwa mshangao.
"I think some times life is always unfair,' alimjibu baada ya kukatiza kicheko chake, "no matter how you try your best, you can always be on wrong side."
****
Alipofika ndani ya lango la majengo yake, aliegesha gari karibu na ofisi yake akashuka kwa utaratibu. Jua lilikuwa lishachomoza likayapa yale manthari rangi ya chungwa, aliangalia saa yake akiinua mkoba wake kwa mkono mwingine na kuanza kuondoka.
"Nilifikiri nimechelewa, lakini nimefika kwa masaa," alijiambia akifikia kicha cha funguo mfukoni mwake, "hongera bwana Nadama."
Alipofunga ofisi yake hakuamini macho yake, vyombo vyote ndani vilikuwa vimebadilishwa, kila chombo cha zamani kilikuwa kimeondolewa na kubadilishana na kipya.
Alisimama mlangoni akiangalia, akatikisa kichwa. Kilichomtoa imani ni zile trey zilizokuwa mezani, trey ya "kutoka" ilikuwa tupu ilhali ya "kuingia" ilikuwa imejaa mpaka ikatapika makaratasi mengine mezani.
"Ni maana kwamba sijafika hapa kwa muda mrefu," aliwazia akiinuka kutoka kitini. Alipofika kalenda kuangalia alipoweka alama, aligundua zilikuwa zimepita wiki tatu kama hajafika ofisini.
Alirudi kitini kuanza kazi iliyokuwa imerundikana mezani lakini hata hakuweza, alishika kalamu lakini akashindwa kuandika. Hata mwenyewe hakujielewa, aliona ni kama katika ubongo wake pamewekwa filamu, alikuwa anakumbuka hili, mara akajipata amelisahau na kuanza kufikiria kwingine.
"Sir, here is your newspaper," katibu wake alimwambia akimkabidhi.
"Asante Gloria," alimshukuru akiliweka chini.
Gloria alimwangalia mkubwa wake kwa sekunde kadha kisha akaanza kuondoka, kwa ghafla alisimama na kumgeukia.
"Jana nilipokea simu kutoka Ujerumani," Gloria alimpa taarifa akifika mbele yake.
"Walitaka Nini?," Mwenzake alimuuliza kwa tamaa.
"Walitaka kufanya nawe biashara ya kuuza magari."
"Hilo ni wazo zuri, tunaweza kufanya nao biashara madhali wawe watu wa kuaminika."
"Ni kweli usemayo," Gloria alimuunga mkono, "walitaka uingie nao katika mkataba ambayo kabla hujafanya dili yoyote unafaa kulipa millioni kuwapa mwanga."
Bw. Nadama aliacha kupekuapekua gazeti akamwangalia Gloria kwa macho ambayo ni kama alikuwa anaanza kutia shaka, Gloria naye alimwangalia lakini moyoni alikuwa ameshtuka. Mkubwa wake alimkataza kwa ishara ya kichwa.
"Hebu fikiri," Bw. Nadama alitamka kuvunja kimya kilichotanda mle ndani, "hao wanaweza kuwa na nia ya kututapeli. Hao ni matapeli, unaezaje kuitisha kiasi hicho cha fedha hata kama hatujaweka makualiano yoyote."
"Lakini bosi unakosea," Gloria alimpinga, "sifikiri kama ni matapeli, kutoka nilipopata mwaliko wao, nimewachunguza mpaka hata kwa mitandao ya kijamii nikakuta kongamano hilo lipo."
"Utandawazi umetupotosha kabisa. Unafikiri kwamba kila kipatikanacho mitandaoni ni kweli...no...hapana. Hata kama kuna kampuni kama hiyo, hatuwezi kutambulika kwake."
Gloria alifikia pochi lake akatoa karatasi alilokuwa amechapisha kuhusu wale waliokuwa wanazungumza akamkabidhi, Bw. Nadama alifikia miwani iliyokuwa mezani akavalia na kuanza kusoma lile karatasi alilokabidhiwa na taarishi wake.
Jina la kampuni likikuwa limeandikwa kwa herufi kubwa kama GRT COMPANY, kisha chini yake picha za magari tofautitofauti. Aliangua kicheko kilichomshitua mwenzake.
"Have you noticed something?," Gloria alimuuliza kwa uoga.
"Ndiyo, kampuni hii ipo Ujerumani ila haina bawa lolote hapa nchini. Hutumia alama ya reli kama kitambulisho chake wala si hiki kisalaba."
Gloria alipokuwa ameketi alifunika kinywa kwa mikono yote miwili akitokwa na machozi.
"Am sorry sir," alimuomba msamaha.
"Msamaha wa nini?."
"Hasara ambayo ningekusababishia."
"Lakini tumegundua mapema mchezo wao, so you don't have to be sad," Bw. Nadama akimsitisha kilio.
"Thank you sir," Gloria alimshikuru akiinuka tayari kuondoka.
Bw. Nadama alimwangalia alivyokuwa anaondoka akaona hapatakuwa na ubaya wowote akimshukuru kwa kazi nzuri aliyokuwa amefanya kutoka alipoondoka ofisini humo. Alikuwa anafikiri labda baada ya kutoitembelea kwa muda wa siku nyingi atapata imechakaa na vumbi kuzagaa kotekote lakini ilikuwa tofauti.
"Gloria..."
"Naam," aliitika akigeuka na kumwangalia, "kila kitu kipo sawa, usiwe na shaka."
"Nimetaka kukupa pongezi kwa kazi nzuri ambayo umefanya humu," Bw. Nadama alimwambia, "kila kitu kipya, ofisi yenyewe umeitunza vizuri."
"Ni kazi yangu boss."
"Sasa ningekuwa mumeo," Bw. Nadama alitamka kumpima kama ni kirukanjia, "ungeninadhifu kwa kiasi hiki!"
"Ah! Hujajua kwamba una wake wawili," Gloria alimwambia akicheka, "Bi. Tabasuri ni mkeo wa nyumbani, nami hapa kazini ni mkeo wa pili. Nafanya kazi kwangu."
"Ni kweli."
Gloria alimwangalia bosi wake kwa macho ya kulegeza kisha akaanza kuondoka, Bw. Nadama alipokuwa alimuona kama mtu aliyemfaa pakubwa sana katika kazi zake za pale ndani, alimuona mwanamke asiyeogopa kusema kilicho akilini mwake.
Sifa hii ya ujasiri ndiyo ilifanya akachaguliwa walipokuwa wanatafuta kazi. Alikuwa mwenye utani na ambaye angeweza kumuondolea mawazo yeyote, alikuwa mwenye maneno mengi kama chiriku, lakini alikuwa akichanganua na kuchagua maneno yake asitamke lolote la kumuudhi yeyote.
"Gloria," alimuita tena.
"Naam," aliitika lakini kwa sauti nzito.
"Nishakuudhi!" Bw. Nadama alimuuliza kwa sauti ya ukarimu.
"La," alikata lakini ni kweli yaliyokuwa yamesemwa.
"Nilikuita kukuarifu kwamba nataka twende ziara, iwe kama zawadi kwa kazi yako nzuri."
"U...na...sem...a ziara!" Gloria alimuuliza kwa kusitasita.
"Ndiyo, nataka kukupeleka ziara ya siku tatu katika mojawapo ya visiwa vilivyoko mashariki mwa Afrika, sijui utachagua kipi; Mombasa, Pate, Lamu au Zanzibar!"
"Asante," Gloria alitoa shukrani akiruka kwa furaha, "chochote utakachochagua."
"Natumai baada ya juma moja utakuwa tayari."
"Hata ikiwa kesho," Gloria alimrukia na kumbusu shavuni, kisha akarudi nyuma kwa haraka akijua amemuudhi, "am sorry!"
"Usitie shaka, nakuelewa."
Aliinama kama njia ya kutoa shukrani kisha akaanza kuondoka, alipofikia komeo ya mlango alisita akageuka na kumwangalia bosi wake. Alimuona akiwa ameshika kichwa chake kuonyesha kifikra alikuwa mbali.
"Sir," Gloria alimgusa baada ya kumsogea, "what about your family? Will they give us company!"
"Kwani una shaka moyoni?," Bw. Nadama alimuuliza akijaribu kupaka uso tabasamu la kulazimisha, "nilifikiri hii ni ziara yetu wawili, lakini ukiona ni heri, basi tutaandamana sote."
"Sina shaka ila namjali Bi. Tabasuri na bintiye, hiyo ziara ya siku tatu ni ndefu."
"Nitafanya utakavyo."
"Utakuwa tayari kupokea simu yoyote kwa leo?," Gloria alimuuliza alipoona hali yake, "unaonekana mwenye mawazo."
"La, leo nina kazi nyingi ya kushughulikia. Nenda uendelee na kazi yako."
"Sawa boss."
Gloria aliondoka akamuacha akipekuapekua gazeti alililomletea. Alisikia sauti ya mkong'oto wa viatu vya taarishi wake vikigonga sakafuni kwa mbali. Like gazeti alikuwa amekodolea macho lakini ungemuuliza yaliyokuwemo hangekujibu, alikuwa akijaribu kufikiri ripoti ambayo alikuwa amepata. Hata Gloria naye katika ofisi yake hakutulia baada ya kuona mwajiri wake katika hali ya kusumbuka.